Tunda linavyoweza kukurudisha katika ujana
Tumekuwa tukiulizwa sana swali hili linalohusu matunda. Wasomaji wetu wengi wamekuwa wakitaka kujua namna nzuri ya kula, lakini wengi wakiwa tayari wanajua kwamba matunda na mbogamboga ndiyo vyakula vinavyomfaa zaidi binadamu, wamekuwa wakitaka kujua namna nzuri ya kula matunda. Wengi wetu tunaposikia kula matunda tunadhani ni kuyatafuta au kuyanunua na kuyakatakata halafu kuyatumbukiza mdomoni, kuyatafuna na kuyameza. Hivyo kwa kweli siyo, kwani kuna utaratibu unaofaa wa ulaji wa matunda. Tumeona litakuwa ni jambo la busara iwapo tutakuelezea namna bora ya kula matunda, ili upate faida zaidi ya ulaji huo. Kuna watu wanaokula matunda baada ya chakula. Hili ni kosa kubwa sana. Matunda yanapaswa kuliwa au kunywa kwenye tumbo tupu, yaani wakati mtu akiwa na njaa. Mtu ambaye anaweza kula tunda kwenye tumbo tupu na kabla ya mlo mkuu, anaweza kufaidika zaidi na ulaji huo wa matunda kuliko yule anayefanya kinyume chake. Hebu tuchukulie kwamba ni asubuhi ambapo umekula vipande viwili vya mkate...